Makamu wa Rais,Dk Mohamed Bilal akizindua rasimu ya katiba mpya |
Chadema kimepinga kauli ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba kuhusu hatima ya Uchaguzi Mkuu wa 2015 kikisema mchakato wa sasa wa Mabaraza ya Katiba, usiwe kikwazo cha mjadala wa muundo wa Serikali Tatu.
Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Chadema, John Mnyika
alisema Dar es Salaam jana kuwa hatima ya Uchaguzi Mkuu wa 2015
utakaotokana na mchakato wa mabadiliko ya Katiba unaoendelea, siyo suala
la kusubiri.
Akizungumza na mwandishi wetu juzi kuhusu kauli ya
Waziri wa Katiba na Sheria Mathias Chikawe kwamba endapo mapendekezo ya
Serikali Tatu yatapitishwa, kuna hatihati ya Uchaguzi Mkuu wa 2015
kufanyika, Jaji Warioba alisema: “Tuachieni muda… hayo mengine ni hisia
tu. Ni kweli tunayajua lakini acheni tumalize hili kwanza ( la Mabaraza
ya Katiba). Hii ndiyo hatua tuliyopo sasa.”
Lakini jana Mnyika alisema: “Hatuwezi kusubiri
hadi Mabaraza ya Katiba yakamilishe mchakato kama alivyoeleza Jaji
Warioba katika gazeti lenu la Mwananchi toleo la leo, (jana),” alisema
Mnyika kwa simu.
Jaji Warioba alitaka suala la muundo wa Serikali
Tatu utakavyokuwa lisiwe hoja kwa sasa kwa kuwa Tume ya Mabadiliko ya
Katiba inachokifanya ni kukusanya maoni kupitia Mabaraza ya Katiba na
kisha kuandaa rasimu itakayopelekwa bungeni kwa ajili ya majadiliano na
kwamba mjadala huo utawachanganya wananchi endapo utaingizwa katika
hatua hii ya ukusanyaji maoni.
Lakini Mnyika alisema: “Mijadala hii haiwezi
kusubiri mpaka hatua ya Mabaraza ya Katiba, inapaswa kuanza wakati huu
kupitia mabaraza yanayosimamiwa na Tume na Mabaraza yanayoendeshwa na
makundi ya kijamii. “Pia, masuala hayo ya mpito pamoja na marekebisho ya
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, ni mambo ambayo yanapaswa kutolewa
ufafanuzi wa ziada na Serikali zaidi ya kauli ambayo Waziri wa Sheria na
Katiba Mathias Chikawe ameitoa kupitia gazeti la lenu la leo (jana).”
Alisema kimsingi bado kunahitajika mjadala wa
masuala ya mpito kwa sababu kuna uwezekano kwamba Katiba Mpya, ya
Muungano au ya Zanzibar na ya Tanganyika, isiwe tayari kabla ya Uchaguzi
Mkuu wa 2015, endapo suala la Serikali tatu litapita.
Alisema kwa upande mwingine, rasimu ya Katiba
iliyotolewa imeibua mjadala juu ya mkwamo wa kikatiba (constitutional
stalemate), ambao ni muhimu upatiwe suluhisho akisema chama chake
kinapendekeza mchakato wa Katiba Mpya ya Tanganyika uanze mara moja ili
uende sambamba na huu wa Katiba Mpya ya Muungano. Alisema ilikuwa vyema
yote yakajadiliwa katika Bunge la Agosti 27, mwaka huu.
Waziri Chikawe alikaririwa na gazeti hili juzi
akisema: “Uwepo wa Serikali tatu utafumua mfumo mzima wa utendaji ndani
ya Serikali. Hatuwezi tena kufanya uchaguzi wa Rais na wabunge 2015,
hatuwezi kufanya chochote nje ya Katiba ya Serikali Tatu kwa kuwa
kinachofuata ni kuunda Katiba nyingine inayohusiana na Serikali tatu.
Waziri Chikawe afafanua
Juzi, Waziri Chikawe alitoa ufafanuzi juu ya utata
wa hoja zake kwa kuipongeza Tume ya Jaji Warioba kwa kazi inayofanya
huku akisema anaunga mkono msimamo wa CCM wa kutaka kuendelea na muundo
wa Muungano wa Serikali mbili.
Alisema mchakato wa kuandika Katiba Mpya unapaswa kuangaliwa kwa jicho pana zaidi ya lile la Uchaguzi Mkuu wa 2015.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
Post a Comment