Licha ya kuwepo kwa sera, sheria, kanuni na vyombo mbalimbali
vya usimamizi na utatuzi wa migogoro ya ardhi hapa nchini, bado migogoro
hiyo inaendelea kuzikabili jamii nyingi za Watanzania, hasa waishio
vijijni.
Sheria ya Ardhi, namba 4 na 5 ya mwaka 1999
hutajwa kuwa sheria bora kabisa katika ukanda wa Afrika Mashariki kwa
kuweka utaratibu mzuri wa umilikaji na uendelezaji wa ardhi, hasa baada
ya kufanyiwa marekebisho mwaka 2004 ambapo iliipa thamani ardhi tupu.
Utekelezaji wa sheria hii na kanuni zake, hasa
katika ardhi za vijiji umegubikwa na kasoro nyingi za kiutendaji ambazo
zimesababisha kuwapo kwa migogoro mingi.
Si kusudio la makala haya kuelezea suala la
migogoro ya ardhi kwa ujumla wake. La hasha! Makala haya yatajikita
kujadili namna ambavyo migogoro ya ardhi maeneo ya shule inavyoathiri
maendeleo na ustawi wa shule kiuchumi na kitaaluma.
Kati ya Februari 2012 na Aprili 2013, nilipata
fursa ya kutembelea baadhi ya shule za msingi au kukutana na wadau wa
elimu ya msingi katika wilaya za Arusha, Iramba, Kigoma, Muleba, Kilwa,
Liwale, Masasi, Mkuranga, Musoma, Ukerewe na Serengeti. Wakati wa
mazungumzo walisema ardhi za shule ni moja ya changamoto zilizoibuliwa
na wadau hao ambao walisema kamati za shule hutumia muda mwingi kutatua
migogoro hiyo badala ya kushughulikia masuala ya maendeleo ya kitaaluma.
Migogoro ya ardhi ya shule, ambayo husababishwa na
ushirikishwaji mdogo wa wananchi katika uamuzi wa kutwaa maeneo ya
shughuli za maendeleo, husababisha uhusiano mbaya baina ya shule na
jamii. Jambo hili husababisha kupungua kwa ari ya wananchi kuchangia
maendeleo ya shule.
Kukiwa na mgogoro, ardhi husika haitumiki hadi
ufumbuzi utakapopatikana, hali inaikosesha shule fursa ya kutumia eneo
husika kwa kazi iliyokuwa imepangwa.Migogoro hiyo ambayo inazikumba hasa
shule zilizoanzishwa hivi karibuni, hufanya wajumbe wa kamati za shule
na baaadhi ya walimu kutumia muda mwingi kuhudhuria kesi katika mabaraza
ya ardhi muda ambao ungetumika kwa shughuli za maendeleo ya shule na
ufundishaji.
Kwa mfano, Shule ya Msingi Ruhobe iliyopo wilayani
Kigoma Vijijini ni moja kati ya shule zinazokabiliwa na migogoro hiyo.
Shule hii ambayo ilianzishwa mwaka 2004 baada ya kugawanywa kutoka shule
mama ya Mwandiga mpaka sasa haina kabisa viwanja vya michezo kutokana
na eneo lililotengwa kwa ajili ya shughuli hiyo kuvamiwa na kugeuzwa
mashamba na baadhi ya wananchi. Kukosekana kwa viwanja vya michezo
kunawanyima fursa waalimu kuibua vipaji vya michezo na kuwajenga watoto
kiafya kwa kufanya mazoezi. Pia kama inavyofahamika michezo sio tu
huimarisha afya ya mwili bali pia huimarisha uwezo wa kufikiri.
Kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi ya Vijiji namba 5 ya
mwaka 1995, utawala wa ardhi ya kijiji uko chini ya mamlaka ya
Halmashauri ya Kijiji. Katika usimamizi wa ardhi ya kijiji, Halmashauri
ya Kijiji haipaswi kugawa ardhi bila ridhaa ya Mkutano Mkuu wa Kijiji.
Shule nyingi za msingi zipo katika ardhi za
vijiji, ni jukumu la halmashauri husika kufuata sheria na kanuni katika
kutwaa ardhi kwa ajili ya matumizi ya shule ili kuepusha migogoro.
Shule ni mali ya jamii, hivyo wanajamii wanao
wajibu wa kuhakikisha ustawi wa maendeleo ya shule kiuchumi na kitaaluma
kwa kuandaa mazingira rafiki ya kutolea elimu ikiwemo kuepusha migogoro
ya aina yoyote itakayoweza kukwaza utoaji wa elimu.
Elisante Kitulo ni Ofisa Program Idara ya Maelekezo na Uongozi; anapatikana kwa barua pepe ya media@hakielimu.org
Post a Comment