0
IKIWA ni siku mbili zimepita tangu tasnia ya muziki wa taarabu hapa nchini kumpoteza mkurugenzi, mtunzi na mpiga kinanda mahiri wa kundi la East African Melody, Haji Mohamed, mchana wa jana imepata pigo tena la kumpoteza nguli mwingine, Fatuma Baraka ‘Bi. Kidude’.



Akizungumzia kifo cha nguli huyo, mwanae Abdallah Baraka alisema marehemu mama yake alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kisukari kwa muda mrefu hadi umauti unapomkuta akiwa nyumbani kwake Bububu mjini Zanzibar.


Baraka alisema mama yake siku kadhaa zilizopita hali yake haikuwa shwari na kuwalazimu kumpeleka hospitalini mara kwa mara kwa ajili ya kuangalia afya yake ambayo ilikuwa ikiwapa wasiwasi hadi jana majira ya saa 7 mchana umauti ulipomkuta.


“Mama yangu alikuwa anasumbuliwa na kisukari kwa muda mrefu, ila siku za hivi karibuni hali yake haikuwa nzuri na kumkimbiza hospitalini mara kwa mara ili kupata matibabu, lakini imeshindikana kwani Mungu amependa zaidi,” alisema Baraka na kuongeza kuwa marehemu atazikwa leo saa 7 mchana katika makaburi ya Kitumba visiwani humo.

Bi. Kidude alikuwa gwiji wa muziki huo na kutamba barani Afrika na nje kutokana na umahiri wake wa kutumbuiza jukwaani vibao vyake mbalimbali kikiwamo ‘Muhogo wa Jang’ombe’.


Muziki huo ambao ni mchanganyiko wa muziki toka nchi za Kiarabu na vionjo vya muziki wa Kiafrika, umejikita sana katika mwambao wa pwani ya Afrika Mashariki.

Bi. Kidude alizaliwa Kijiji cha Mfagimarigo Unguja katika familia ya watoto saba, ambako baba yake Mzee Baraka alikuwa ni mfanyabiashara wa nazi, zao ambalo ni la kutumainiwa Zanzibar.


Bi. Kidude aliwahi kusimulia kuwa hafahamu tarehe halisi aliyozaliwa, isipokuwa anachojua ni kwamba alizaliwa wakati rupia ikitumika kama fedha. Wataalamu wa mahesabu baada ya kupata taarifa hizo wakampigia mahesabu na kumkabidhi miaka yake kwamba ni zaidi ya miaka 100.

Katika historia yake enzi za uhai wake, Bi. Kidude alisema uimbaji aliuanza tangu alipokuwa na miaka 10 na alijifunza kutoka kwa msanii mkongwe na aliyetamba sana enzi hizo, Sitti binti Saad.


Anasema wageni wengi kutoka sehemu mbalimbali walikuwa wakifika Zanzibar kumwona Sitti, na kwa vile walikuwa wako karibu, basi alikuwa akiwapeleka wageni wale nyumbani kwake, na wakifika huko walikuwa wakiingia ndani na yeye kubakia nje.

Huko ndani, Bi. Sitti alikuwa akiwaimbia wale wageni na yeye akiwa nje akimsikiliza kwa makini, akimuigiza jinsi alivyokuwa akiimba na kutumia nafasi hiyo ambayo ilimfanya kupata umaarufu zaidi hadi akawa mahiri sana katika uimbaji.

Alipokuwa na miaka 13, kwa mara ya kwanza alitoroka nyumbani kwao Zanzibar na kukimbilia Tanzania Bara, baada ya kulazimishwa kuolewa.


Lakini alipokuwa kigoli wa kutosha kuolewa, aliolewa ingawa ndoa hiyo nayo haikudumu kutokana na manyanyaso aliyokuwa akiyapata, hivyo aliamua kukimbilia kaskazini mwa Misri ikiwa ni katika miaka ya 1930, ambako huko aling'ara sana katika fani yake ya uimbaji na uchezaji ngoma.

Lakini ilipofika miaka ya 1940, aliamua kurudi nyumbani Zanzibar ambako aliendelea na shughuli zake za uimbaji.

Bi. Kidude enzi zake, alikuwa hategemei kazi moja tu ya kuimba, kwani pia ni mfanyabiashara ya wanja na hina ambavyo anavitengeneza yeye mwenyewe. Pia ni mtaalamu wa matibabu kwa dawa za miti shamba na zaidi ya hayo ni mwalimu mzuri sana wa unyago na alianzisha chuo chake mwenyewe na anasema katika wanafunzi wake wote, hakuna aliyepata talaka kutoka kwa mumewe.

Post a Comment

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...
 
Top