Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimeamua kuachana na kuwania umeya
wa Jiji na badala yake kimemwomba Meya, Gaudence Lyimo (CCM), atende
haki.
Katibu
wa Kanda ya Kaskazini wa chama hicho, Amani Golugwa alisema jana,
kwamba Chadema haina uroho wa madaraka kama baadhi ya watu
wanavyofikiri, bali inasimamia vipaumbele vya maendeleo.
Hata
hivyo, kauli hiyo inapingana na nyingine ya chama hicho ya wiki hii
pia, kwamba ushindi katika uchaguzi mdogo wa kata nne, ni chachu katika
msimamo wa chama kutaka uchaguzi wa Meya wa Jiji la Arusha, urudiwe.
Mwenyekiti
wa Madiwani wa Chadema, Isaya Doita, ndiye aliyenukuliwa wiki hii
akisema hayo, akiamini kuwa Meya Lyimo wa CCM, alichaguliwa kimizengwe.
Baada ya
Chadema kutetea viti vyake vinne vya udiwani kwenye uchaguzi mdogo wa
hivi karibuni, kimefikisha viti 15 kwenye Baraza la Madiwani la Arusha,
huku CCM ikibaki na viti 12 na TLP sita.
Pia
Chadema ina nafasi ya kuongeza kiti, kwani ina nafasi moja ya viti
maalumu iliyokuwa inakaliwa na Rehema Mohamed, aliyetimuliwa mwaka 2011.
Hata
hivyo, pamoja na Chadema kuongoza kwa kuwa na viti vingi vya udiwani
jijini hapa, haina uwezo wa kuweka Meya, bila kushirikiana na CCM au
TLP.
Chadema
ikikosa ushirikiano huo, ushirikiano wa CCM na TLP, utabaki kuwa na
nguvu ya kuweka Meya na naibu wake madarakani, huku Chadema ikibaki kuwa
kambi ya upinzani yenye nguvu katika Baraza la Madiwani.
Golugwa
alisema Chadema haina uroho wa madaraka, bali inataka uchaguzi wa Meya
wa Jiji urudiwe ingawa haitaki nafasi hiyo kwa kuwa si kipaumbele chake.
"Tunaangalia
wananchi wanafikiwaje na maendeleo tuna imani muda si mrefu Jiji la
Arusha litapata Meya ambaye amechaguliwa kwa misingi ya sheria," alisema
Golugwa.
"Hatuna
shida na Meya wala hatuna uroho wa madaraka tunachopinga ni upatikanaji
wa Meya huyo na tunamtaka afanye kazi zake kwa kusimamia misingi ya
sheria na si upendeleo, tunahitaji kuona kila mwananchi ananufaika na
maendeleo hadi mitaani," aliongeza.
Pia
alikaririwa wakati mmoja akisema ushindi huo unaihakikishia Chadema
wingi wa wajumbe katika Baraza la Madiwani, hivyo kuwa na fursa ya
kumwondoa Lyimo madarakani.
Post a Comment