Utamaduni
wa taasisi nyingi hapa nchini wa kukataa kuwajibika pale makosa
yanapofanyika, badala yake lawama zikaelekezwa mahali pengine
pasipohusika, sasa unaonekana kama jambo la kawaida. Ni utamaduni hasi
wa kutokubali kuwajibika kwa jambo lolote linalokwenda kombo, badala
yake kuwanyooshea vidole watu wengine, tena ambao hawahusiki katika
kusababisha matatizo hayo.
Ni
utamaduni huo ambao umefifisha dhana ya uwajibikaji katika nchi yetu.
Ni utamaduni unaojenga mazingira ya mtu kutaka sifa pale mambo
yanapokwenda vizuri, hata kama hukuchangia lolote katika kuleta hali
hiyo ya mafanikio. Yanapotokea matatizo, hulka ya wengi ni kuruka
kimanga na kusema sio wao.
Tunaweza
kusema kwamba hakuna chombo kilichoathiriwa na utamaduni huo hapa
nchini kama Serikali. Mhimili huo wa dola ndio umefanywa kama gunia la
kufanyia mazoezi ya ndondi kwa kugeuzwa kisingizio cha kila tatizo
linalojitokeza. Hapana ubishi kwamba yapo matatizo yanayosababishwa na
mhimili huo.
Lakini,
aghalabu mhimili huo umekuwa hautendewi haki, kwani hata watendaji wake
wanapohusika kufanya uamuzi fulani, wanakuwa wa kwanza kuelekeza lawama
kwa mhimili huo pindi uamuzi walioufanya unatoa matokeo yasiyokubalika.
Mifano
ni mingi, lakini kutokana na ufinyu wa nafasi katika safu hii, tutatoa
michache tu ya matukio ya hivi karibuni. Hatua ya chama tawala (CCM),
ambacho juzi kilitoa taarifa ya kuilaumu Serikali kwa kuweka tozo ya
Sh1,000 kwa kila laini ya simu ya kiganjani imewaacha wananchi wengi
wakiwa midomo wazi. Hii ni kutokana na ukweli kwamba chama hicho
kilikuwa nyuma ya Serikali katika kufanya uamuzi wa kuweka tozo hiyo.
Baada ya tozo hiyo kupingwa na wananchi ndipo chama hicho kilipoamua
kuruka kimanga kwa malengo ya kisiasa.
Yafaa
tukumbuke hapa kwamba tozo hiyo ilipitishwa na Bunge katika kikao cha
Bajeti mwezi uliopita wakati pia liliporidhia Sheria ya Fedha. Serikali
ilipeleka mapendekezo kuhusu tozo hiyo na ilikuwa juu ya Bunge
kuyakubali au kuyakataa. Zaidi ya theluthi mbili ya wabunge wanatoka CCM
na ukweli ni kwamba ndio haohao waliopitisha Bajeti ya Serikali na
mapendekezo yake kuhusu tozo ya laini za simu. Hatua ya chama hicho
kuilaumu Serikali baada ya tozo hiyo kupingwa na wananchi ni kutoitendea
haki katika kutaka kujinusuru kisiasa.
Utamaduni
wa kutowajibika wakati matatizo yanapotokea pia jana ulidhihirishwa na
Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia, Januari Makamba aliposema wizara
yake haikubaliani na tozo hizo. Inashangaza kuona viongozi wa wizara
hiyo wanapingana na dhana ya uwajibikaji wa pamoja, kwani tozo hiyo
imewekwa na Serikali ambayo wao ni watumishi wake. Ni mwendelezo wa
utamaduni wa kuruka kimanga hata kama nao walishiriki katika chombo
kilichoamua kuanzisha tozo hiyo inayopingwa na wananchi.
Ni
utamaduni ambao sasa umejikita katika jamii yetu. Undumilakuwili huo
tunaoshuhudia katika suala la tozo ya laini za simu ndio tulioshuhudia
katika matukio mengi huko nyuma, likiwamo la Sheria ya Mifuko ya Hifadhi
za Jamii ambayo ilipitishwa na Bunge kwa msukumo wa idadi kubwa ya
wabunge wa CCM, lakini wakaruka kimanga kwa malengo ya kisiasa baada ya
sheria hiyo kupingwa kila kona ya nchi. Ndio maana tunasema katika hili
la tozo ya laini za simu, Bunge ndilo libebe lawama badala ya Serikali.
Post a Comment