0


Kikao cha Bunge la Jamhuri ya Muungano, mjini Dodoma.
Nchi masikini za Afrika ikiwamo Tanzania zinatumia fedha nyingi kulipa wabunge wakati utendaji kazi wa viongozi hao wa kisiasa ni mdogo na hauendani na marupurupu na mishahara minono wanayolipwa, utafiti  wa REPOA umebaini.
Katika utafiti huo, imegundulika kuwa wakati kada ya wabunge inalipwa fedha nyingi katika nchi zenye uchumi unaokua kwa kuchechemea, wananchi na watumishi wengine wa Serikali wameachwa wanaogelea katika dimbwi la umasikini.
Utafiti huo ambao umefanywa na Dk Ted Valentine umebaini kuwa nchi za Afrika Mashariki ndizo zinatumia fedha nyingi kulipa wanasiasa kuliko hali halisi ya uchumi wa nchi hizo, hali inayotia wasiwasi kuwa huenda zikashindwa kuhimili kulipa mishahara hiyo minono kutokana na uchumi wao mdogo.
Dk Valentine wa Kenya katika utafiti wake alioubatiza jina la Afrika inaweza kumudu gharama za Demokrasia katika kuwalipa Wabunge’, alisema Kenya inaongoza kulipa wabunge wake, Uganda ya pili na Tanzania ya tatu katika nchi za Afrika Mashariki.
Wakati nchi masikini za Afrika zikipigana vikumbo kulipa wanasiasa mishahara minono, nchi za Ulaya kama Norway na Ufaransa ni miongoni mwa nchi zinazolipa fedha kidogo wanasiasa wakiwamo wabunge huku watumishi wengine wakilipwa vizuri.
Wabunge kulipwa mishahara hiyo mizuri kumeelezwa na mtafiti huyo kuwa kunatokana na wabunge wenyewe kuruhusiwa na Katiba zao kujipangia na kupitisha mishahara, hali inayowapa fursa ya kujipendelea.
Kwa sasa pato la Mbunge nchini Kenya ni mara 140 ya pato la mtumishi wa kawaida wa Serikali wakati Tanzania pato hilo ni mara 40 ya pato la mtumishi wa kawaida.
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba ameshauri kiwepo chombo maalumu huru kitakachokuwa kinapanga mishahara ya watumishi wote wa Serikali wakiwamo viongozi wa nchi, wabunge na  watumishi wengine serikalini.
Alisema kwa kuwa Tanzania iko kwenye mchakato wa kuandika Katiba mpya, ni vema chombo hicho kiainishwe katika Katiba hiyo ili kuepuka wanasiasa kukiingilia au kukishinikiza. "Tukiwa na taasisi huru inayopanga mishahara naamini itazingatia hali halisi ya uchumi na kipato cha wananchi wa kawaida."

Profesa Lipumba ambaye ni mchumi, alishauri mapato ya wabunge yasiwe tofauti na ya watumishi wengine wa Serikali. Pia alisema mishahara ya viongozi wa kisiasa isiwe siri kama ilivyo sasa, ambapo  wananchi hawajui mishahara ya viongozi wao wakiwamo wabunge.
"Wananchi wana haki ya kujua viongozi wao wanalipwa kiasi gani, nchi zingine ikiwamo Canada, mishahara ya viongozi iko hata kwenye tovuti ya Serikali, hakuna usiri, lakini hapa kwetu hakuna uwazi katika kupanga mishahara hiyo," alisema Profesa Lipumba.
Kuhusu hoja ya uwajibikaji wa wabunge, Profesa Lipumba alikubaliana na hoja ya Dk Valentine na akatoa mfano kuwa kuna fedha zilitengwa na kutumiwa na Wizara ya Nishati na Madini katika kujenga kinu cha kufua umeme Mtwara, lakini mradi huo haukufanyika.
Alisema licha ya kuwapo kasoro hiyo, hakuna mbunge ambaye alihoji suala hilo na akasema inadhihirisha jinsi wabunge wasivyofanya utafiti wa namna ya kuisimamia Serikali. Alisema kuna haja ya kuwawezesha wabunge ili wawe na uwezo wa kuisimamia Serikali.
Mkurugenzi wa Repoa, Dk Samuel Wangwe alisema wabunge wamekuwa wanajipendelea  kujipangia mishahara, lakini umefika wakati sasa kada hiyo ilipwe mishahara inayokwenda na ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Alisema pia kwamba baadhi ya wabunge licha ya kulipwa fedha nyingi hivyo, hawawajibiki katika kuisimamia Serikali na akashauri wajipime waone kama wanawajibika kulingana na kipato chao.

Post a Comment

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...
 
Top