0


Johannesburg. Mamia ya wananchi wa Afrika Kusini jana walifurika kwenye Hospitali ya Medi-Clinic, Pretoria alikolazwa Rais wa Kwanza mzalendo wa nchi hiyo, kuimba wimbo wa ‘Happy Birthday’ kuadhimisha siku yake ya kuzaliwa.

Licha ya baridi kali, wakazi hao wakiwamo wanafunzi wa shule, vyuo wakiwamo zaidi ya 100 wa kile cha Nelson Mandela, taasisi na waumini wa madhehebu mbalimbali walikusanyika kuanzia saa 12 asubuhi nje ya hospitali hiyo, kumwimbia Mandela huku baadhi wakiwa wameshika mabango yenye maneno mbalimbali ya kumtakia uponaji wa
haraka na kumpongeza kwa kutimiza miaka 95. Alizaliwa Julai 18, 1918 katika Kijiji cha Mvezo, Jimbo la Cape.

Kadi mbalimbali ziliwekwa katika ukuta wa hospitali hiyo pamoja na maua na zawadi ambavyo baadaye vilikusanywa na kupelekwa Kituo cha Kumbukumbu ya Mandela.

Siku hiyo ya kuzaliwa kwa kiongozi huyo pia ni sikukuu ya kimataifa inayojulikana kwa jina la ‘Mandela Day’ maalumu kwa ajili ya kuenzi na kukumbuka mchango wa shujaa huyo wa Afrika katika kutetea haki za binadamu na kupinga ubaguzi wa rangi.

Katika maadhimisho hayo, raia wa Afrika Kusini walitumia dakika 67 kufanya kazi za jamii. Dakika hizo zimekokotolewa katika muda ambao alianza harakati za kisiasa, kipindi kufungwa na uongozi kwa taifa hilo kuanzia mwaka 1942 hadi alipostaafu rasmi mwaka 2009. Rais Jacob Zuma alimtembelea Mandela hospitalini hapo jana mara baada ya kutimiza dakika zake 67 za kufanya kazi za jamii kwa kukabidhi nyumba 407 kwa Wazungu wanaoishi katika makazi duni ya Bethlehemu karibu na Pretoria.

“Nawaomba watu wa Afrika Kusini wote kusherehekea kwa furaha siku hii. Ni vizuri kila mtu akatimiza ahadi kwa kuzitumia dakika zake 67,” alisema Zuma. Askofu Mkuu wa zamani wa Kanisa la Anglikana Afrika Kusini, Desmond Tutu alimuenzi Mandela kwa kusaidia kupaka rangi Shule ya Msingi ya Marconi Beam, Joe Slovo nje kidogo ya Cape Town.

Apata kitambulisho

Miongoni mwa matukio ya kipekee yaliyoinakshi siku hiyo ni pamoja na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Afrika Kusini kumkabidhi Mandela, kitambulisho kipya cha uraia ambacho kilipokewa kwa niaba yake na mtoto wake, Zindzi.

Vitambulisho hivyo vipya kwa Waafrika Kusini vinatolewa kwa mara ya kwanza na vitatumika katika uchaguzi wa Rais na wabunge mwakani.

Mara baada ya kupokea kitambulisho hicho kwa niaba ya baba yake, Zindzi alisema anafurahi kuona baba yake amekuwa miongoni mwa watu wa kwanza nchini humo kupata kitambulisho hicho. “Nitakwenda kumpa baba kitambulisho chake na nina hakika atafurahi. Tunashukuru watu wote kwa jinsi wanavyomthamini baba yetu Madiba,” alisema Zindzi.

Watu wengine wa kwanza kupata vitambulisho hivyo ni kizazi cha wazee walioshiriki katika harakati za ukombozi wa Afrika Kusini akiwamo Rais wa zamani wa nchi hiyo, FW de Klerk, Makamu wa Rais, Kgalema Motlanthe, Rais wa zamani, Thabo Mbeki, Spika wa zamani, Frene Ginwala, Sophie de Bryun ambaye aliwaongoza wanawake katika ukombozi mwaka 1956.

Huko Mamelodi, mashariki mwa Pretoria, wajukuu wa Mandela, Ndileka, Tukwini, Ndaba na wanafamilia wengine walishirikiana na kituo cha watoto yatima kuwakabidhi chakula watoto wanaoishi katika mazingira magumu sambamba na kupanda miti.

Post a Comment

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...
 
Top