LICHA ya kuwapo kwa shutuma mbalimbali zinazopinga mpango wa
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuanzisha kikundi cha
kujihami cha Red Brigade kitakachotoa ulinzi kwa viongozi wao,
imebainika kuwa msajili wa vyama vya siasa nchini, John Tendwa alitoa
baraka za kuanzishwa kwake.
Tanzania Daima imeona nakala ya barua ya mwaka 2005 kutoka katika
ofisi ya Tendwa, ikionyesha kubariki jambo hilo ambalo katika siku za
hivi karibuni limezua gumzo kubwa na kusababisha Mwenyekiti wa CHADEMA,
Freeman Mbowe, kuhojiwa na polisi kuhusiana na kauli zake.
Uchunguzi wa kina uliofanywa na Tanzania Daima umebaini kuwa Desemba
30, 2004 ofisi ya msajili wa vyama siasa ilimwandikia Katibu Mkuu wa
CHADEMA barua yenye kumbukumbu Na. RPP/CHADEMA/72/29 ikitaka ufafan
uzi
baada ya kusikia kupitia vyombo vya habari kuwa chama hicho kinataka
kuanzisha kikundi cha kujihami (Red Brigade).
“Kulingana na Ibara ya 9 (2) (c) ya Sheria Na. 5 ya Vyama vya Siasa
1992, ibara ya 147 na 148 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
na Sheria ya Jeshi la Polisi, kuanzishwa kwa kikundi hicho ni kinyume
cha sheria hizo,” imeeleza sehemu ya barua hiyo.
Barua hiyo ambayo Tanzania Daima inayo iliyosainiwa na Hilda Lugembe
kwa niaba ya msajili wa vyama vya siasa, inaeleza kuwa kuvunjwa kwa
sheria hizo kutasababisha CHADEMA kufutwa.
CHADEMA baada ya kupata barua hiyo, Januari 6 mwaka 2005 iliijibu
kuwa kikundi kinachozungumziwa ni walinzi wa ndani ya chama, vijana wa
kike na wa kiume, wanachama wa CHADEMA, watu wasio na silaha, chini ya
usimamizi wa kurugenzi ya ulinzi na usalama ya chama hicho.
“Kikundi kinachokusudiwa kuundwa ni kutokana na Katiba ya CHADEMA
ambayo inaruhusu uundwaji wa Kurugenzi ya Ulinzi na Usalama chini ya
Katiba ya CHADEMA, kifungu cha 7.6.4 (h),” inaeleza barua ya CHADEMA
yenye kumbukumbu Na. C/HQ/ADM/64 iliyosainiwa na Suzan Kiwanga kwa
niaba ya Katibu Mkuu wa CHADEMA.
Chama hicho kiliilaumu serikali kwa vitisho ilivyotoa vya kutaka
kukifuta endapo kingeendelea na kusudio la kuanzisha kikundi hicho.
Hata hivyo, baada ya ufafanuzi huo, Januari 11 mwaka 2005, ofisi ya
msajili wa vyama vya siasa, ilipopata majibu hayo ya CHADEMA, ilieleza
kuwa kwa madhumuni yaliyoelezwa na chama hicho inakubaliana na malengo
ya kuanzisha kikundi cha ulinzi kwa ajili ya usalama wa ndani ya chama.
“Ofisi ya msajili wa vyama vya siasa, kwa madhumuni mliyoyatoa kwenye
barua yenu C/HQ/ADM/62 inakubaliana na maelezo yenu ya kuanzishwa kwa
kikundi cha ulinzi kwa ajili ya usalama wa ndani ya chama ingawa Katiba
ya CHADEMA haijatoa ufafanuzi huo, vinginevyo tunawatakia kila la heri
kwenye matayarisho ya uundwaji wa kikundi hicho,” ilisema barua ya
msajili wa vyama vya siasa nchini.
Barua hiyo yenye kumbukumbu Na. RPP/CHADEMA/72/32 iliyosainiwa na
Hilda Lugembe kwa niaba ya msajili wa vyama vya siasa nchini, pia
iliwatakia kila la heri CHADEMA kwenye matayarisho ya uundwaji wa
kikundi hicho.
Nakala za majibu ya Ofisi ya Tendwa kwa CHADEMA zilipelekwa kwa
Waziri wa Mambo ya Ndani wakati huo, Omar Mapuri, Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Waziri Mkuu, aliyekuwa anashughulikia Habari na Siasa, Muhammed
Seif Khatib; Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu; Inspekta Jenerali wa
Polisi na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai.
CHADEMA waibua mjadala
Julai 9 mwaka huu akisoma maazimio ya Kamati Kuu ya CHADEMA mbele ya
vyombo vya habari, Mwenyekiti wa chama hicho, Mbowe alitangaza mpango
wa kuboresha vikundi vya mafunzo ya kujilinda.
Baada ya kauli hiyo watu mbalimbali akiwemo Rais Jakaya Kikwete,
walijitokeza kuupinga mpango huo kwa madai kuwa utasababisha uvunjivu
wa amani na utulivu vilivyodumu kwa muda mrefu hivi sasa.
Ofisi ya msajili wa vyama vya siasa pia alimwandikia barua Katibu
Mkuu wa CHADEMA yenye kumbukumbu Na. 112/123/16A/3 kukitaka chama hicho
kuacha kutekeleza mpango huo kwani kufanya hivyo ni kukiuka sheria za
nchi ikiwamo sheria ya vyama vya siasa ya mwaka 1992 hali inayoonyesha
kujikanganya kwa ofisi hiyo kwani awali ilisharuhusu kitu hicho.
Barua hiyo kutoka ofisi ya msajili inaongeza kuwa; “Kifungu cha 9(2)
(c) cha sheria ya vyama vya siasa kinakataza chama cha siasa kuruhusu
kutumika, kushabikia au kutumia nguvu na vurugu ili kufikia malengo
yake ya kisiasa.”
Kwa mujibu wa barua hiyo iliyosainiwa na Sisty L. Nyahoza kwa niaba
ya Msajili wa Vyama vya Siasa, madai ya CHADEMA kusema kuwa “Chama Cha
Mapinduzi (CCM) wana kambi za mafunzo ya kupambana isiwe kisingizio
cha vyama vingine vya siasa kuvunja sheria ya vyama vya siasa.”
Msajili pia kupitia barua hiyo amesema “kama CCM wanakiuka sheria, ni
jukumu la CHADEMA, kila chama na kila Mtanzania kutoa taarifa na
ikiwezekana na ushahidi katika taasisi husika ikiwamo ofisi ya msajili
wa vyama vya siasa ili suala hili lishughulikiwe kisheria.”
Hata hivyo, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa katika majibu
yake aliifahamisha Ofisi ya Msajili kuwa matumizi ya nguvu ikiwamo
silaha kwa ajili ya ulinzi wa maisha au mali yameruhusiwa na sheria ya
jinai kanuni ya adhabu sura ya 16 ya sheria ya Tanzania.
“Nimeshangazwa sana na kauli yako kwamba vikundi vya ulinzi vya vyama
vya siasa vinapaswa kuwa na wanachama wasiokuwa na mafunzo ya kijeshi
au ukakamavu kama ilivyo kwa walinzi wa majumbani, kauli hii
inadhihirisha ufahamu wako mdogo wa mambo haya.
Kwanza walinzi wa
majumbani na maofisini wanaoajiriwa na utitiri wa kampuni binafsi za
ulinzi zilizosajiliwa nchini kwetu hupatiwa mafunzo ya ulinzi na
ukakamavu na wengine hupatiwa silaha za moto,” alisema Slaa.
Alisema kauli hiyo ya msajili wa vyama vya siasa kwamba jukumu la
vikundi vya ulinzi si kupambana na wahalifu au watu wanaotaka
kuwadhuru, ni hatari sana kwani inawapotosha wananchi wasitumie haki
yao ya kujilinda wanaposhambuliwa au kudhuriwa na wahalifu wa kisiasa.
“Barua yako inatutishia kwamba endapo tutatekeleza mpango wetu wa
mafunzo kwa kikundi chetu cha ulinzi utakuwa si uamuzi wa busara kwa
uhai wa chama chetu.
“Kwa maneno mengine endapo tutatekeleza haki yetu ya kujilinda kama
tunavyoruhusiwa na sheria za nchi yetu, kama tulivyoeleza katika barua
hii, utatumia mamlaka yako kumaliza uhai wetu kama chama cha siasa kwa
kufuta usajili.
Hatutaki kuamini kwamba na wewe pia unatumiwa na CCM
kukandamiza na kutoa vitisho kwa chama kingine kwa manufaa yake,”
alisema Dk. Slaa. CHANZO TANZANIA DAIMA.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post a Comment